German Ambassador Writes Farewell  Letter to Kenyans in Swahili

Andreas Peschke, Omer Othman; Prof. Peter Mbithi
File photo of Amb. Andreas Peschke during an event at the University of Nairobi. Looking on are Omer Othman and Prof. Peter Mbithi

Nilipokuja Kenya kwa mara ya kwanza 1993 kama mwanachuo, sikufikiri kuwa, baada ya miaka 20, nitarudi kama Balozi wa Ujerumani nchini Kenya. Sasa kazi yangu kama balozi itamalizika. Lakini urafiki wangu kwa Kenya na wananchi wa Kenya utabaki.

Kenya imefika mbali tangu uhuru. Katika mambo ya kibiashara na kiuchumi, Kenya inaongoza eneo zima la Afrika Mashariki. Wataalamu na waandishi wa Kenya ni mashuhuri duniani kote. Kenya inajitolea sana pia katika mambo ya mabadiliko ya hali ya hewa na kukabiliana na uwindaji haramu. Tena taifa la Kenya liko mbele katika kupiga vita ugaidi.

Kenya inabarikiwa na urithi mkubwa wa kiutamaduni. Wananchi wa Kenya wana nguvu na uwezo mwingi. Hakuna nchi nyingine katika eneo la Afrika ya Mashariki ambayo ina jamii wazi na huru kama Kenya. Nilienjoy sana mbinu za habari nyingi tena huru na utumiaji mkubwa wa mitandao ya kijamii nchini Kenya. Hii ndiyo misingi ya uhuru ambayo inasukuma nchi mbele. Nafikiri kuwa Wakenya wana sababu nyingi za kujivunia nchi yao.

Wakenya walipopitisha katiba yao mpya mwaka 2010, Wajerumani wengi walifuata hatua hiyo kwa makini sana. Kwa sababu, Ujerumani pia ndiyo nchi yenye ugatuzi mwingi. Katika historia yetu, tunajua changamoto na nafasi za ugatuzi wa madaraka na fedha. Siyo kazi rahisi na tena inahitajika kila siku jitihada kubwa kutatua shida na mizozo mbalimbali kati ya viwango tofauti vya serikali. Lakini sisi tulijifunza kitu kimoja: Ugatuzi hutoa fursa nzuri sana ya kuleta utawala karibu na watu.

Ushirikiano kati ya Kenya na Ujerumani ni mkubwa sana. Tulishirikiana tangu Ujerumani ilipokuwa taifa la kwanza kutambua rasmi taifa la Kenya baada ya uhuru 1963. Leo tuko marafiki ambao wanasaidiana na kuheshimiana.

Ninafurahi sana kuwa ushirikiano wetu katika biashara na uwekezaji umeongezeka sana. Nilipofika hapa Shirika la Biashara la Kijerumani lilikuwa na wanachama 90. Leo idadi yao imeongezeka kuwa zaidi ya 130. Kampuni kubwa kutoka Ujerumani kama Bosch ama Merck zilifungua ofisi mjini Nairobi, nyingine kama vile Daimler ama Allianz zinatarajia kufanya hivyo hivi karibuni. Kampuni ya BASF ilifungua kiwanda kipya mjini Nairobi mwaka uliopita. Kampuni yetu ya ndege Lufthansa itaanza safari kati ya Frankfurt na Nairobi mwezi wa kumi. Ushirikiano wetu unaleta faida kwa nchi zetu mbili. Kwa mfano, kampuni kutoka Ujerumani zinaunga mkono pia juhudi za Serikali ya Kenya za kuongeza nafasi za mafunzo ya ufundi nchini Kenya ili kuwapatia vijana nafasi zaidi za kujiendeleza.

Kuhusu ushirikiano wa maendeleo, Ujerumani na Kenya zinashirikiana katika kilimo, kutoa maji safi na huduma za afya. Tunashirikiana pia katika sekta ya uzalishaji wa umeme kutumia kawi ya mvuke wa kutoka ardhini katika Bonde la Ufa, nishati ya upepo kutoka kando ya ziwa la Turkana ama kawi ya jua. Lengo letu la pamoja ni kutekeleza mipango ya Serikali ya Kenya ya kuongeza sana uzalishaji wa umeme. Tunashirikiana pia kujenga, kurekebisha na kukarabati shule za msingi maeneo kadhaa ili kuwapa wanafunzi mandhari mema ya kusomea.

German Ambassador to Kenya, Andreas Peschke speaking SwahiliGuess who was spotted speaking swahili…..mmmhhmmm the German ambassador to Kenya, Andreas Peschke

Posted by Mkenya Ujerumani on Sunday, January 18, 2015

Kiswahili kufundishwa Ujerumani

Katika fani ya utamaduni, tunashirikiana ili watu wa tamaduni, lugha na dini tofauti tofauti wazidi kufahamiana na kuelewana. Wanachuo elfu mbili wanasoma lugha ya Kijerumani kwenya Idara yetu ya Goethe jijini Nairobi kila mwaka. Kila mwaka, Tamasha la Utamaduni na lugha ya Kijerumani huleta pamoja wanafunzi 1000 kutoka pembe zote za Kenya wanaoshiriki katika mashindano ya kuigiza kwa lugha ya Kijerumani. Kiswahili ambayo ndiyo lugha ya taifa ya Kenya inafundishwa katika vyuo vikuu saba nchini Ujerumani. Shirika letu la kuunga mkono wanachuo DAAD lina wanachuo wa zamani 10,000 nchini Kenya na Afrika Mashariki. Katika Shule ya Kijerumani jijini Nairobi wanafunzi 300 kutoka Kenya, Ujerumani na mataifa mengine wanasoma pamoja.

Tunashirikiana sana pia katika usalama. Ujerumani inatathmini sana mzigo mkubwa ambao unabebwa na Kenya katika mapambano dhidi ya ugaidi. Zaidi ya ushirikiano wetu na polisi na jeshi, Ujerumani iliwapatia ufadhili wa kimasomo wanachuo 300 walionusurika shambulio la kigaidi kwenye Chuo Kikuu cha Garissa ili waweze kuendelea na masomo yao. Hii inaonyesha wazi: Lazima tusimame pamoja na kusaidiana katika vita dhidi ya uovu huu wa ugaidi.

Kwa hivyo, Kenya na Ujerumani zina uhusiano wa urafiki na ushirikiano wa karibu sana. Nilifurahi sana kuishi hapa Kenya na kufanya kazi ili kuimarisha uhusiano kati ya nchi zetu. Kenya ndilo taifa lenye nguvu na uwezo kubwa. Nitawakosa sana marafiki wetu nchini Kenya. Nikiondoka nasema: Kwaheri ya kuonana!

Tukutane tena.

Share with friends:

1 Trackbacks & Pingbacks

  1. New German Ambassador to Kenya Named | Mkenya Ujerumani

Comments are closed.